KISA KIPYA CHA EBOLA CHARIPOTIWA HUKO SIERRA LEONE.

                 Kisa kipya cha ugonjwa wa Ebola kimeripotiwa huko nchini Sierra Leone, na hii inaashiria kuwepo kwa hatari ya kutokea maambukizi mapya, hii ni kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO.
Kisa hiki kimejitokeza wakati shirika la afya WHO limetangaza kumalizika kwa maambukizi ya Ebola huko Liberia na Guinea. Kisa hiki kipya ni kiashiria kuwa mapambano dhidi ya maradhi haya hatari ya Ebola bado hayajamalizika.
Katika waraka uliotolewa jana(14 Januari 2016) na WHO, shirika hilo limesisitiza kuwa nchi za Liberia, Sierra Leone na Guinea, bado zitakuwa katika hatari ya kupata maambukizi mapya katika miezi ijayo kwa sababu bado virusi hivi viimeendelea kubaki katika mifumo ya mwili ya manusura walioambukizwa maradhi haya hapo awali.
Nchi ya Sierra Leone bado ipo katika uangalizi madhubuti wa siku 90 tangu ilipotangazwa kumalizika kwa maambukizi ya virusi vya Ebola mnamo tarehe 7 Novemba 2015. Muda huu ulitengwa maalum ili kuhakikisha kuwa kuwa hata virusi vilivyojificha katika mifumo ya mwili vinang'amuliwa ili kukomesha kabisa maambukizi ya Ebola.

Comments